Monday, 10 October 2016

LISHE YA KUKU NA KUCHANGANYA CHAKULA

Image result for chicken food mixing

 LISHE YA KUKU:
Ili kuku waweze kuishi, kukua vizuri, kunenepa na kutaga mayai mengi ni lazima wale chakula kingi na chenye ubora unaotakiwa. Uwingi na ubora wa lishe ya kuku unaweza kuainishwa katika makundi ya vyakula kama ifuatavyo:
1.      Vyakula vya kutia nguvu
2.      Vyakula vya kujenga mwili
3.      Vyakula vya kuimarisha mifupa
4.      Vyakula vya kulinda mwili
5.      Maji.

Makundi ya vyakula:

    1. Vyakula vya kutia nguvu:
Vyakula vya mifugo vifuatavyo vinawekwa katika kundi hili;
a.       Pumba za mahindi, pumba laini za mpunga, na, pumba laini za ngano.
b.      Nafaka kama vile mtama , chenga za mahindi ,chenga za mchele, uwele , na ulezi
c.       Mimea ya mizizi kama vile muhogo, viazi vitamu na magimbi. Kabla ya kulisha kuku hakikisha mizizi hiyo inalowekwa kwa muda wa saa moja au kupikwa kabla ya kukausha ili kuondoa sumu ambayo kwa asili imo katika vyakula vya aina hii.Inashauriwa kuwa  mizizi hiyo ilishwe kwa kiasi cha asilimia 10% ya chakula chote anacholishwa kuku.
 Katika kundi hili la kutia nguvu ,vyakula vya mafuta kama vile mafuta ya kutoka kwenye vyakula vya mafuta kama mashudu ya mimea ya mafuta, mafuta ya samaki husaidia kuongeza nguvu na joto mwilini. Vyakula vya kutia nishati huchangia asilimia 60-70 ya mchanganyiko wote wa chakula.
1.        Vyakula vya kujenga mwili:
Ø  Mashudu :Haya ni makapi ya mbegu za mimea aina ya mikunde na vyakula v vinavyotoa mafuta kama vile alizeti, mawese, karanga, soya ,korosho, na ufuta .
Ø  Damu ya wanyama iliyokaushwa (waliochinjwa na kukaguliwa), hii inafanywa ili kuepusha uwezekano wa kuku kupata magonjwa ya kuambukiza .
Ø  Mabaki ya samaki ya samaki/dagaa na nyama.
Ø  Vyakula asilia kama vile minyoo, mayai ya mchwa, Masalia ya nyama toka kwenye ngozi/mifupa, wadudu walioteshwa kutokana na damu au nyama iliyooza na vyakula vya aina nyingine.
Ø  Vyakula hivi huchangia asilimia 20 hadi 30% ya mchanganyiko wote wa chakula cha kuku.
2.   Vyakula vya kuimarisha mifupa(madini): a)Hivi ni vyakula vya madini ambavyo huhitajika kwa ajili ya kujenga mifupa, maganda ya mayai, kukua na kuuweka mwili wa ndege (kuku) katika hali ya afya njema kwa ujumla.
b)      Madini ya muhimu ni madini ya chokaa (calcium) na fosiforasi (phosphorus). Ili kuku watage mayai yenye ganda gumu ni lazima wapate madini ya chokaa maganda ya konokono na mayai yaliyosagwa vizuri. Lakini inapendekezwa kwamba unapoongeza madini ya fosforasi inakubidi uongeze pia madini ya chokaa kadri inavyopasa ,kwasababu kiwango cha aina moja kikizidi kuliko cha aina nyingine husababisha upungufu wa kile kidogo
Viinilishe vya madini vinavyotakiwa ni pamoja na;
Ø  Majivu ya mifupa yaliyosagwa vizuri, unga uliosagwa wa magamba ya konokono wa baharini, konokono wa nchi kavu na maganda ya mayai yaliyochomwa . Kabla maganda ya mayai na nyumba za konokono havijatumika inashauriwa yachomwe moto mkali au yachemshwe ili kuua vijidudu vya maradhi.
Ø  Chumvi ya jikoni
Ø  Madini yaliyotengenezwa viwandani kama vile Di-calcium phosphate
Ø  Magadi (kilambo).
 4.      Vyakula vya kulinda mwili:
Kundi hili linajumuisha vyakula vya mbogamboga kama vile;
Ø  Mchicha, samadi ya ng’ombe ambayo haijakaa muda mrefu baada ya kunyewa, mchicha pori, Chinese kabeji n.k.
Ø  na Mchanganyiko wa vitamini uliotengenezwa na viwanda vya madawa (vitamin premix).
Ø  Jua ni muhimu katika kuhakikisha vitamini A na D zinatumika vizuri mwilini, kwahiyo banda ni lazima lijengwe kwa mtindo ambao unaruhusu mwanga kupita hasa nyakati za asubuhi na jioni.
Ø  Chakula cha kuku wanaofugwa ndani ni lazima kichanganywe na vitamini zinazotayarishwa viwandani.

          KUCHANGANYA CHAKULA CHA KUKU:

Njia za kuchanganya chakula cha kuku;
Kuna njia kuu mbili za kuchanganya chakula cha kuku, nazo ni;
Ø  Kuchanganya chakula kwa mashine;
o   Njia hii hutumika viwandani kuchanganya chakula kwa ajili ya kuku wanaofugwa katika mashamba makubwa.
Ø  Kuchanganya chakula majumbani (home made ration): Hii ni njia inayotumika kuchanganya chakula kwa ajili ya kulisha kundi dogo la kuku na njia ambayo inaweza kutumiwa na wafugaji wadogowadogo.
VIFAA; Beleshi /koleo(spade), Turubai/sakafu safi, Viinilishe , Viroba/Magunia kwa ajili ya kuhifadhia chakula kilichochanganywa.
Chakula kilichochanganywa kinaweza kuwekwa katika uzani wa kilo 25-kilo 50, au kilo 100.
                MCHANGANUO WA VIINILISHE VYA CHAKULA CHA KUKU:

 
Aina ya chakula                                   kiasi
i.                    Vyakula vya kutia nguvu mwilini:
Ø  Pumba za mahindi            kilo   48
Ø  Pumba laini za mpunga    kilo   26
            Jumla                                            kilo 74
  ii.            Vyakula cha kujenga mwili : 
                                       

    Mashudu ya alizeti                                   kilo 18

        Damu ya wanyama                                                                    kilo   1
        Mabaki ya samaki /dagaa                                                          kilo   3

          Jumla                                              kilo  22

iii.Vyakula vya kuimarisha mifupa (Madini):
  1. chumvi ya jikoni                                   kilo ½
  2. chokaa(dicalciumphosphate)…            kilo 2
  3. poultry premix/                                     kilo ½ 
  4.  unga wa mifupa                                  kilo 1
          Jumla                                                      kilo 4
  
Ø  Mahitaji halisi ya viinilishe kwa muhtasari:
Ø  Vyakula kutia nguvu mwilini                             kilo 74
Ø  Vyakula vya kujenga mwili                              kilo 22
Ø  Vyakula vya kuimarisha mifupa (Madini)        kilo 4
  JUMLA                                                                        100
Jumla ya mchanganyiko wa vyakula                kilo 100 

 

HATUA ZA KUCHANGANYA CHAKULA CHA KUKU:

HATUA YA KWANZA:
Katika hatua ya kwanza utaanza kuchanganya vyakula vya madini
Changanya , chokaa, chumvi na majivu ya mifupa pig mix vizuri - huu utauita mchanganyo Na.1
HATUA YA PILI:
Changanya mchanganyo huo na damu pamoja na samaki waliosagwa - huu utauita mchanganyo Na. 2
 HATUA YA TATU:
Mchanganyo Na.2 uchanganye na mashudu vizuri ambao utauita mchanganyo Na.3.
HATUA YA NNE:
Mchanganyo Na.3 umwage juu ya rundo la pumba iliyochanganywa (pumba ya mahindi na pumba laini ya mpunga).
o   Chukua beleshi /koleo safi lililo kavu na kulitumia kuchanganya rundo la chakula ili kusambaza viinilishe vizuri.
Mambo ya kuzingatia katika kulisha na kutunza chakula cha kuku:
a) Baada ya kuchanganya chakula kitawekwa kwenye viroba au magunia na kutunzwa ghalani (stoo) hadi pale kitakapohitajika kwa ajili ya kulisha kuku.
b) Hakikisha kuku wanapata lishe kadri inavyopendekezwa na wataalamu.
c)  Chakula kilichochanganywa ni lazima kiwekwe sehemu kavu ili kisiharibiwe na unyevunyevu kama vile kwenye chaga mabanzi yaliyotandazwa juu ya mawe yalipangwa vizuri
d)  Chakula kilichoharibika hakifai kulisha kuku kwani kinaweza kusababisha matatizo ya afya.
d) Chakula kilichochanganywa kinatakiwa kisikae muda mrefu baada ya kutayarishwa.
Vyakula vya ziada:
Ili kuhakikisha kwamba kuku wanapata viinilishe vya kutosha kuku wanaweza kupewa mchwa na mafunza.
Vilevile vitu mbadala aina ya nafaka vinavyopatikana hutegemea sana aina ya mazao yanayolimwa katika eneo husika.
Mbinu za kuotesha mchwa na funza: Funza na mchwa ni chakula kizuri na rahisi chenye viinilishe aina ya protini kwa kuku wanaofugwa kwa mfumo huria unaoboreshwa. Hata hivyo vyanzo hivi vya chakula cha protini huchangia tu vile ambavyo kuku wanatakiwa kupewa.
a.       Inashauriwa uwape vifaranga hao funza na mchwa kwa sababu ndio wanaohitaji protini kwa kiasi kikubwa na cha kuaminika.
Funza na mabuu yanaweza kuoteshwa kwa njia rahisi na kutumika kuboresha chakula cha vifaranga.
      c)   Mafunza na mabuu yanaweza kuoteshwa kwa kutumia damu, viungo vya ndani ya tumbo la ng’ombe pamoja na samadi ya ng’ombe.
d)   Chungu kijazwe maji theluthi moja ya ujazo wake, inzi watakuja na kutaga mayai katika mchanganyiko ambao mafunza walioteshwa wataanza kula mchanganyiko huo.
e)   Baada ya hapo vitu hivi vyote vitachanganywa pamoja katika chungu kimoja kikubwa ambacho kitaachwa wazi wakati wa mchana na kufunikwa wakati wa usiku.
f)    Siku tano baadaye maji yatajazwa kwenye mtungi huo na mafunza yatakusanywa wakiwa wanaelea juu. Baada ya kukusanya waoshe vizuri na maji halafu lisha kuku moja kwa moja.
g)   Kumbuka kuweka chungu kinachooteshwa mafunza kuweka mbali na maeneo ya watu ili kuepuka harufu inayoweza kusumbua watu.
                                                  KULISHA KUKU:  
 
 Makadirio ya chakula cha kuwalisha vifaranga 100/siku moja:
Umri (wiki baada ya kuzaliwa)
Idadi ya
 vifaranga
Kiasi kinachotakiwa
Kwa siku moja(kilo)
1
100
1
2
100
1
3
100
2
4
100
3
5
100
4
6
100
5
Maelezo kwa ufupi  kuhusu kulisha kuku:
§  Ni vigumu kukadiria mahitaji ya chakula cha kuku wanaojitafutia chakula, lakini inakadiriwa kuwa kuku mmoja mkubwa wa uzito wa kilo 1-2 anahitaji chakula chenye uzani wa gramu 80-160 kwa siku kwa kuku wanofugwa ndani lakini wale kuku wanafugwa kwa mfumo wa huria nusu huria mahitaji yanakadiriwa kupungua hadi kufikia gramu 30-50 kwa siku .
§  Ifahamike pia kuwa kiasi cha chakula hutegemea mahitaji kutokana na uzito na uzalishaji, mfano kuku anayetaga na anayekua wanahitaji chakula kingi zaidi ya wale ambao hawatagi au wamekoma kukua.
§  Hakikisha kuku wanawekewa chakula na maji safi kwenye vyombo safi na kubadilisha kila vitakapoisha.

ushauri zaidi Wasiliana nasi @kukuproject 
 Whatsapp (0715-908307 ,0653-691138) au tupigie kwa 07169-457675,0678226498

Wednesday, 5 October 2016

FAHAMU SIFA ZA BANDA BORA LA KUKU

Image result for CHICKEN HOUSE

Sifa za banda bora la Kuku
Ukiamua kufuga katika banda kwa njia mbili zilizoelezwa awali utatakiwa kujenga banda lenye sifa zitakazokidhi mahitaji ya msingi ya kuku. Banda bora la kuku linatakiwa kuwa kama ifuatavyo: Ready more>>
Liwe jengo imara
• Pasiwe na sehemu zilizo wazi kwenye msingi na kati ya ukuta na paa.
• Banda lijengwe na vifaa vinavyopatikana katika mazingira yako ili liwe na gharama utakayoweza kumudu.
• Unaweza kutumia matofali ya udongo, udongo, miti, fito,n.k. Ukitumia fito au mabanzi ondoa maganda ili kuthibiti mchwa.
• Jengo mara litazuia maadui kama panya, vicheche, paka, nyoka na wezi kuingia ndani ya banda na kuwadhuru au kuwaiba kuku.
Liwe rahisi kusafisha
• Kuta na sakafu visiribwe zisiwe na nyufa ili kurahisisha kusafisha.
• Pia itadhibiti kusiwe na wadudu wa kujificha katika nyufa kama papasi, viroboto n.k.
• Sakafu ya banda lazima iwekewe matandazo kama pumba ya mpunga au maranda ya mbao au mabaki ya mazao au nyasi kavu kutegemeana na kinachopatikana kwa urahisi katika mazingira yako.
• Matandazo haya husaidia kunyonya unyevu unaotokana na kinyesi cha kuku au maji yanayomwagika katika banda.
• Banda hubakia kavu bila kuwa na harufu mbaya na wadudu kama inzi hata vimelea vya magonjwa hudhibitiwa.
Eneo la nje kuzunguka banda kuwe na usafi wa kudumu
Hali ya usafi nje ya banda itafanya wadudu kama siafu au mchwa na wanyama kama panya na paka mwitu wakose maficho. Nje ya banda ndani ya uzio kuwe na miti midogo na mimea mingine midogo kwa ajili ya kivuli.
Ufugaji nusu huria
Banda liwe na nafasi ya kutosha kwa kuku waliopo: Kwa kawaida eneo la mita mraba moja hutosha kuku wanne wanaotaga au kuku 8 wa nyama. Nafasi ya mita mraba 1 inatosha vifaranga 16 hadi kufikia umri wa majuma manne.
Liweze kuingiza hewa na mwanga wa kutosha: Banda linaloweza kuingiza hewa safi na kutoka ndani yake hubaki kavu. Harufu mbaya hutoka na kuku huweza kupumua hewa safi. Hii husaidia pia kudhibiti kuzaliana kwa vimelea vinavyosababisha magonjwa,hivyo hudhibiti magonjwa.
Lisiwe na joto sana au baridi sana: Panda miti ya kuzunguka banda lako ili eneo liwe na kivuli cha kutosha na pia lisiwe na upepo mkali.Kama hali halisi ya eneo la kufugia ina joto kubwa kwa vipindi virefu paa la banda wakati wa ujenzi liinuliwe juu zaidi kuruhusu mzunguko zaidi wa hewa na joto la paa ( kama ni la bati) liwe mbali juu ya kuku.
Joto kwenye banda linaweza kusababishwa na msongamano wa kuku, hivyo mfugaji aangalie aweke idadi ya kuku inayowiana na ukubwa wa banda lake.
Paa
Liwe imara na lisilovuja. Waweza kutumia mabati, nyasi, madebe, makuti n.k. kutegemeana na upatikanaji wa vifaa vya kuezekea.Wakati wa kuezeka paa lisiishie karibu sana na ukuta bali liwe na sehemu kubwa iliyozidi ukuta kuzuia mvua kuingia ndani kama ni ya upepo ( angalia mchoro hapa chini).
Vifaa vinavyohitajika katika banda la kuku
Kuku wakifugwa kwa mtindo wa nusu ndani na nusu nje wanahitaji huduma mbalimbali ndani ya banda na ndani ya wigo. Ili kutoa huduma hizi vifaa vifuatavyo ni muhimu viwe katika banda:
Vyombo vya Maji
Kuna njia nyingi za kutengeneza vyombo vya kuwekea maji ya kuku ya kunywa.
• Aina ya mojawapo unayoweza kutumia ndoo au debe la lita kumi au ishirini ya plastiki. Kata ndoo hiyo pande nne kutoa nafasi ya kuku ya kunywea kama kielelezo kinavyoonyesha. Tengeneza idadi ya vyombo hivi inayowiana na wingi wa kuku ulionao.
• Au waweza kutumia sufuria au beseni pana kiasi. Hii huwekewa tofali au jiwe safi pana baada ya kuwekewa maji ya kunywa ili kuzuia kuku wadogo wasizame na maji yasichafiliwe kirahisi.
• Vifaa maalum vya kunyweshea kuku vinapatikana katika maduka ya pembejeo za kilimo.
Vyombo vya chakula.
Vyombo hivi ni muhimu viwe vimetengenezwa vizuri ili visiwe chanzo cha upoteaji wa chakula. Unapotengeneza kilishio cha kuku kumbuka kuwa kuku wana tabia ya kuchakura. Husambaza au kupekua chakula kwa miguu hata kwa midomo ili kupata chakula cha chini.
Tabia hii husababisha kumwagwa kwa chakula kingi chini na kusababisha hasara. Unaweza kudhibiti tatizo hili kwa kutengeneza vyombo visivyoruhusu kuku kuchakura kama inavyoonyeshwa kwenye kielelezo hapa chini.
Unaweza kutengeneza kilishio hiki wewe mwenyewe au fundi seremala waliopo katika eneo unaloishi. Inafaa kilishio kiwe chembamba ili kuku wasiweze kuingia. Pia kinatakiwa kiwe kirefu ili kuku waweze kula bila kusongamana.
Viota
Zipo aina tofauti za viota ambazo hutumika kwa ajili ya kutagia. Ipo aina ya ambayo ni ya kutagia kuku mmoja mmoja. Vipimo vinavyopendekezwa kwa kila kiota ni upana wa sentimita 30, urefu sentimita 30 na kina sentimita 35. Upande wa mbele uachwe wazi ila sentimita 10 za kwanza kutoka chini zizibwe na ubao ( angalia kielelezo). Weka idadi ya viota inayotosheleza kuku ulio nao.
Pia ipo aina nyingine inayoweza kutumiwa na kuku zaidi ya mmoja kwa wakati mmoja. Ni kama kiota kimoja kilichogawanywa katika vyumba kadhaa. Ila kila chumba kina vipimo kama vya kiota kimoja( angalia picha hapa chini).Aina hii ya kiota ina upana wa sentimita 30 na kina sentimeta 35 na urefu wake unategemea idadi ya viota.
Viota vinatakiwa kuwa na giza ili kuku wasiogope kuingia kutaga ndani yake. Pia giza husaidia kupunguza tabia ya kuku kula mayai na kudonoana. Kiota kinafaa kuwekwa mahali ambako ni rahisi kuku kuingia na kutoka. Vile vile iwe ni sehemu itakayorahisisha usafishaji wa kiota chenyewe.
Kichanja.
Kuku wana asili ya kupenda kulala au kupumzika sehemu iliyoinuka. Hivyo ndani ya banda weka vichanja vitakavyotosheleza idadi ya kuku waliopo
Ulishaji: Kuku wa kienyeji wanaweza kulishwa kwa kumia mahindi, mchele, na mabaki ya ugali. Vyakula hivi ni lazima vikaushwe vizuri na kusagwa vizuri. Ulishaji ni lazima ufanyike katika sehemu safi au kwa kutumia vyombo vilivyotengenezwa maalumu kwa ajilii ya kulishia kuku. 
Banda: Kuku wawe wa kienyeji au wa kisasa, wanahitaji kuwa na banda zuri kwa ajili ya malazi na kuwalinda. Wanahitaji chumba chenye nafasi ya kutosha na kinachopitisha hewa ya kutosha. Ni lazima kuwawekea fito kwa kuwa ndege hupenda kupumzika juu ya fito. Ni lazima banda la kuku lifungwe vizuri nyakati za usiku ili kuzuia wanyama wanaoweza kuwadhuru kuku. Ni lazima liwe safi wakati wote ili kuzuia magonjwa kama vile mdondo na mengineyo. Usitumie pumba za mbao au nguo kuukuu kwenye viota vya kutagia kwani huchochea kuwepo utitiri na funza wa kuku. Inashauriwa kutumia mchanga laini.
Maji ya kunywa: Kuku wapatiwe maji safi. Ni lazima kuangalia mara kwa mara na kuyabadilisha maji. Kamwe usiwape kuku maji machafu.
Chanjo: Chanjo kwa mifugo ni lazima ili kuzuia mashambulizi ya magonjwa. Magonjwa yaliyozoeleka ni kama vile Mdondo, Kideri, Ndui ya kuku, na homa ya matumbo (typhoid). Chanjo kwa kawaida hutolewa mara moja kwa kila baada ya miezi miwili.
Uwekaji wa kumbukumbu: Kumbukumbu zijumuishe aina ya ulishaji, namba ya uzalishaji, muda wa mwisho wa matumizi, kiasi cha malisho kwa kila siku, idadi ya vifo, na idadi ya mayai yaliyozalishwa.
Mwanzoni unahitaji nini?
Wafugaji walio wengi wanauliza wanahitaji nini katika hatua za awali ili kuweza kuanzisha mradi wa ufugaji wa kuku. Hii itategemea aina ya kuku uliochagua kufuga.
Ni busara kuwa na vifaa muhimu vinavyohitajika na viwe katika hali ya usafi kabla ya kuweka kuku bandani mwako. Kama unaanza na vifaranga, vifuatavyo ni vifaa muhimu vinavyohitajika kwa ajili ya vifaranga 200.
• Tenga na utengeneze banda zuri lenye joto na hewa ya kutosha wakati wote.
• Vyombo vinne (4) vya kunyweshea maji, hii ni katika wiki 2 za mwanzo na uongeze vyombo taratibu kulingana na kuku wanavyokua.
• Vyombo vinne (4) vya kulishia chakula, na viongezeke kulingana na kuku wanavyokua.
• Matandazo makavu na safi, inaweza kuwa maranda au mabua ya ngano.
• Pakiti moja au mbili za dawa ya Coccid (hii inapatikana katika maduka yote ya kilimo). Hata hivyo, utaratibu wa chanjo ni lazima ukamilishwe.

• Chakula kwa ajili ya vifaranga ambacho kimezalishwa na watengenezaji wanaoaminika

Maelezo na ushauri zaidi wasiliana nasi :-

Tupigie kwa namba zetu 0769-457675 na 0678-226478
Au kupitia Whatsapp 0715-908307 na 0653-691138
Kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 11 jioni

Thursday, 29 September 2016

ANZISHA MRADI WAKO WA KUFUGA KUKU LEO

Image result for jinsi ya kufuga kuku

MAHITAJI
  1. Kuku(tetea) 10 na Jogoo 01
  2. Banda bora
  3. Vyombo vya chakula na maji
  4. Chakula bora
  5. Madawa na chanjo kwajili ya magonjwa
  6. Chanzo cha nishati joto na mwanga
  7. Elimu na ujuzi wa malezi bora
  8. Chombo au chumba cha kutunzia vifaranga
  9. Mayai ya kuku wa kisasa/mayai mabovu(ambayo hayakuanguliwa)
  10. Madaftari au kitabu cha kutunzia kumbukumbu
KUKU 10
Wakati wa kuanza mradi wako hakikisha una kuku 10 (matetea) wenye umri sawa na hawajawai kutaga hata mara moja. Chagua kuku wenye rangi nzuri kutoka katika familia bora kutegemea malengo ya mradi wako. Mfano kama lengo lako ni kuzalisha kuku wa kienyeji kwajili ya nyama basi chagua mbegu ambayo inakuwa haraka na yenye uzito mkubwa. Au ikiwa lengo ni mayai basi ni vema kuchagua aina ya kuku yenye kukua haraka na kutaga mayai mengi.
Ili kupunguza gharama za manunuzi ya kuku na hivyo kuongeza faida kwa mfugaji ni vema kununua kuku wadogo ambao wametoka tu kuachishwa kulelewa na mama zao. Kuku hawa utawapata kwa bei ya chini, tena watafaa sana maana watakua na umri mmoja pia.
JOGOO 01
Jogoo mmoja tu anatosha kuwahudumia kuku matetea yote kumi. Hakikisha katika uchaguzi wa jogoo bora lililochangamka, rangi mzuri, upanga umesimama, macho angavu, uzito wa kutosha, rangi nzuri na uwezo mkubwa wa kuzalisha. Ni vema mfugaji akaelewa kwamba kuku wote watakaozalishwa watategemea ubora wa jogoo wake. Uwezo wa kutaga kwa kuku na upatikanaji wa mayai pia hutegemea kwa karibu ubora wa jogoo aliyechaguliwa.
BANDA BORA
Miongoni mwa mambo mhimu naya kwanza kuzingatiwa katika ufugaji wa kuku wa kienyeji kama mradi ni maandalizi ya banda bora. Kuku huhitaji banda bora ili wasiathirike na madhara mbalimbali. Mfugaji anatakiwa kuandaa banda lenye ukubwa wa mita 10 kwa mita 04. Yani urefu uwe mita 10 na upana upana wa mita 04. Kisha kata vyumba vya mita 2 urefu na upana mita 4 kutoka katika banda lako hivyo utakuwa na jumla ya vyumba vitano vyenye ukubwa unaolingana. Ujenzi uzingatie malighafi na vifaa vinavyopatikana kwa urahisi katika mazingira husika. Mfano katika maeneo ambayo fitoKuku zinapatikana kwa urahisi banda linaweza kuandaliwa kwa miti na kukandikwa kwa udongo. Au sehemu ambayo mabanzi hupatikana kwa urahisi basi banda laweza kujengwa kwa kutumia mabanzi. Vifaa vya kujengea banda vizingatie pia gharama na upatikanaji wake katika eneo husika. Baadhi ya vifaa hivyo ni kama ifuatavyo:-
  • Sakafu: Saruji, udongo, mbao, mianzi au fito
  • Kuta: Fito, mabanzi, mbao, nguzo mianzi,udongo, matofali, mawe, mabati na wavu
  • Paa: Nyasi, makuti, majani ya migomba, mabati na vigae.
  • Wigo: Matofali, mbao, fito nguzo, mabanzi, mianzi, matete, wavu na mabati
Banda bora la kuku linatakiwa kuwa na sifa zifuatazo:-
  • Imara, lenye uwezo wa kuwahifadhi kiafya na pia dhidi ya hali ya hewa hatarishi kwa mfano jua kali, upepo, baridi na mvua pamoja na wanyama hatari.
  • Lenye mwanga, hewa na nafasi ya kutosha inayoruhusu usafi kufanyika kwa urahisi.
  • Lijengwe sehemu yenye mwinuko isiyotuama maji, isiyo na upepo mkali na iwe mbali kidogo na nyumba ya kuishi watu.
  • Liwe na vichanja kwa ajili ya kuku kupumzika na kulala.
  • Liwe na sehemu ya kuwekea chakula, maji, kutagia, kuatamia na sehemu ya kulelea vifaranga.
  • Liwe na nafasi ya kutosha kulingana na idadi ya kuku na kuweka vyombo vya chakula na maji.
  • Kwenye mazingira ya joto banda liwe la ukuta mfupi na sehemu kubwa wazi yenye wavu hadi kufikia kwenye paa. Kwenye mazingira ya baridi banda liwe na ukuta mrefu unaokaribia paa na sehemu ndogo tu iwe wazi yenye wavu ili kupitisha hewa na mwanga.
JINSI YA KUFANYA
Wakuze kuku wako hadi watakapofikia muda wa kutaga. Wakianza kutetea ni kiashiria kwamba wakati wa kutaga umekaribia hivyo andaa viota kwajili ya kutagia.
Viota vinapaswa viwe na ukubwa stahiki ili kumwezesha kuku kuyafunika mayai yote vizuri wakati wa kuetamia, viota viwe vinavyozuia mayai kutawanyika, viwe mahali pakavu na safi.
Hakikisha kuku wote wanataga katika viota tofauti. Kuku anapotaga IMG_20140306_153739mayai matatu unapashwa kuchukua mayai mawili na kumwachia yai moja ili kumfanya aendelee kutaga zaidi. Kuku akifikia yai la kumi na mbili anza kumwachia mayai matatu ili kumwandaa kwa kazi ya kuetamia. Kwa kufanya hivi, kuku atataga mayai 15 au zaidi na ikiwa atataga mayai 15 au chini ya hapo nakushauri utafute mayai mengine ujazilizie ili kufikisha mayai 20 kwa kila kuku. Zingatia kwamba mayai unayoyatoa kwa kila kuku, yanatunzwa sehemu salama, mahali pakavu, pasafi na penye joto la wastani.
Kuku wote wanapaswa kuanza kuetamia kwa siku moja. Ili kufanikisha hili inapasa uwe karibu na kuku wako. Kuku mmoja akianza kuetamia mwekee mayai ya kuku wa kisasa au mayai mabovu ya kuku wa kienyeji. Utafanya hivi hadi kuku wako wote watakapoanza kuetamia mayai. Kuweka mayai mabovu au mayai ya kuku yaliyotumika humfanya kuku aendelee kuetamia akijua ni mayai yake.
Baada ya kuona kwamba kuku wako wote wapo tayari kwa kuetamia mayai, waandalie banda maalumu kwajili ya kuetamia yani chumba kimoja katika lile banda letu. Ninashauri kwamba chumba kwajili ya kuetamia kiwe chumba cha kwanza au cha mwisho katika mfuatano wa vyumba vya banda lako. Andaa viota bora vya kuetamia, weka mayai 20 kwa kila kiota, ikiwa hayajatimia unaweza kununua kwa wafugaji wengine ili kuifikia idadi yako.
Waamishe kuku kutoka wanapotagia na kuwaweka katika chumba ulichokiandaa kwajili ya kuetamia. Ili ufanikiwe katika zoezi hili inafaa lifanyike wakati wa usiku na unafanya katika giza. Mweke kuku katika kila kiota na asubuhi wajikute kila mmoja katika kiota chake. Wahudumie kwa chakula na maji ya kutosha. Wakati wa usiku waongezee joto la ziada kwa kuweka jiko au ndoo ya chuma yenye chengachenga za mkaa au kama una umeme weka taa za joto.
Baada ya siku 21-25 kuku wako wataanza kuangua vifaranga. Huu ndio wakati unaotakiwa kuwa karibu sana na kuku wako kuliko wakati wote. Watenge vifaranga mara tu baada ya kuanguliwa; waweke katika chumba chao maalumu mbali na kuku. Kama chumba cha kuetamia kilikuwa cha kwanza basi vifaranga wawe chumba cha mwisho n.k
Ukishawatenga vifaranga mbali na matetea wako, wawekee tena mayai mengine 20 kila tetea, mayai ambayo utayanunua kwa wafigaji wenzako. Hakikisha kuku waliotaga hayo mayai ni wazuri, hawana magonjwa na wanauzito/ukubwa unaofaa. Mayai yote yakaguliwe vizuri ili kujua kwamba yameharibika, yana nyufa au mabovu. Kabla ya kuweka mayai mengine hakikisha chumba chako ni kisafi na viota vimesafishwa, havina wadudu na uchafu wowote. Kuku wako bila kujijua wataanza kuetamia upya mayai uliowawekea.
Ukiwawekea mayai rudia mzunguko kama nilivyokwambia awali. Baada ya siku 21 hadi 25 tena utapata vifaranga wako wengine tena. Fuata kila hatua kama nilivyokwambia hapo awali. Lakini kwa awamu hii nashauri waache matetea wako wapumzike wala usiwapatie mayai mengine tena.
JINSI YA KULEA VIFARANGA
Ikikaribia siku ya 20 tangu ulipowawekea matetea wako mayai katika chumba cha kuetamia, andaa chumba kwa ajili ya kulea vifaranga. Safisha kwa kuondoa uchafu na wadudu wote.
Washa taa ya joto au weka chombo cha kutoa joto katika chumba cha vifaranga nusu saa kabla hujaIMG_20141114_104757anza kuingiza vifaranga wako. Weka pia chakula na maji ya kutosha katika vyombo vyenye umbile na ukubwa utakaowawezesha vifaranga kuvitumia. Tandaza magazeti, maboksi, makaratasi n.k katika sakafu ya chumba hicho. Hakikisha vifaranga wako hawajikusanyi sehemu moja maana wakifanya hivyo wengi wao watakufa ili ufanikiwe katika jambo hili, banda lako liwe la mduara katika kona zake.
Weka joto la kutosha. Joto la kutosha ni lile linalowafanya vifaranga watawanyike chini ya chanzo cha joto wakati kama joto limezidi vifaranya kukimbia mbali na chanzo cha joto na ikiwa joto halitoshi vifaranga hujukusanya chini ya chanzo cha joto.
Baada ya siku 3 utawapatia chanjo ya Gumboro na siku 7 wapatie chanjo ya New Castle, utarudia tena kuwapa chanjo hii baada ya mwezi mmoja kisha utafanya hivi kila baada ya miezi mitatu mitatu.
MAPATO YA MRADI WAKO
Katika uzazi wa kwanza utapata vifaranga 150 kwa wastani wa vifaranga 15 kwa kila kuku. Tuseme haujazingatia kanuni za ufugaji za makala hii ukapata vifaranga 100 yani wastani wa vifaranga 10 kwa kila kuku. Kisha baadaye wakakua wakafa kuku 50 yani watano kwa kila kuku utakuwa na jumla ya kuku 50.
Baada ya wiki 3 utapata tena kuku tufanye kwa mahesabu kama hayo hapo juu kwa hasara utakuwa na kuku wengine 50, na kufanya jumla ya kuku 100. Ikiwa kuku wako baada ya uzao wa pili uliwapumzisha kwa miezi miwili basi mwezi wa 3 utapata tena kuku vifaranga 100 na wiki 3 baadaye utapata wengine 100. Kwa mahesabu kama hayo awali wakikuwa utakuwa na kuku wengine 100 ambao watakuwa.
Baada ya miezi 6 utakuwa na kuku wakubwa wa uzao wa kwanza 50, uzao wa pili kuku 50 na utakuwa na kuku wenye umri wa miezi mitatu 50 wa uzao wa 3 na kuku wengine 50 wa uzao wa 4.
Katika kuku 100 wa uzao wa kwanza na pili, tufanye kuku 50 wawe matetea ukijumlisha na kuku 10 ulioanza nao mradi utakuwa na matetea 60. Ikiwa kila tetea atatotoa vifaranga 10 na vikakua vitano tu, mwishoni utakuwa na kuku 300 na baada ya miezi mitatu kuku wengine 900 toka katika kutoka kwa uzao wa kwanza, wapili na watatu. Hivyo mwaka wa pili utafunga na kuku si chini ya 1,200/= wanaotaga mayai.
Ukiuza majogoo yote 1,200/= kwa bei ya 8,000/= ili upate pesa ya kujenga miundombinu bora maana sasa utakuwa na kuku wengi wanaoendelea kuzaliana kwa kasi utapata pesa kiasi cha TZS 7,200,000/=. Sasa ongeza kuku wako wa kutaga hadi wafikie kuku 4,000 maana sasa utakuwa na pesa za kutosha kuendesha mradi wako.
IMG_20140309_101614Sasa ukiwa na kuku 4000 wa kienyeji wa kutaga mayai, ikiwa kuku 3000 tu watataga ukauza yai moja kwa bei ya haraka haraka ya TZS 250 tu, utapata TZS 750,000/= kwa siku ambayo sawa na TZS 22,500,000/= kwa mwezi na TZS 270,000,000/= kwa mwaka sawa sawa na 128,572 USD. Kumbuka mwamba makadilio haya niya chini sana. Ukifata kanuni zote kwa makini na maombi huku ukimtanguliza Mungu utafikia hata TZS 500,000,000/= kwa mwaka.
Kumbuka unapofanikiwa kupata mapato ya kila aina, umtolee Mungu zaka(x10%) ya mapato yako, pia ukatoe sadaka ambayo ni kubwa kuliko zaka na uwasaidie masikini na wahitaji.
Tunza kumbukumbu zako zote za fedha katika daftari maalumu kuhusu mapato na matumizi ya mradi wako. Pia hali ya kuku wako kuhusu tarehe za chanjo ya mwisho, siku walipoanza kuetamia, magonjwa yanayowasumbua mara kwa mara n.k
Wasiliana nasi kwa maswali, maoni au ushauri.