Wednesday 5 October 2016

FAHAMU SIFA ZA BANDA BORA LA KUKU

Image result for CHICKEN HOUSE

Sifa za banda bora la Kuku
Ukiamua kufuga katika banda kwa njia mbili zilizoelezwa awali utatakiwa kujenga banda lenye sifa zitakazokidhi mahitaji ya msingi ya kuku. Banda bora la kuku linatakiwa kuwa kama ifuatavyo: Ready more>>
Liwe jengo imara
• Pasiwe na sehemu zilizo wazi kwenye msingi na kati ya ukuta na paa.
• Banda lijengwe na vifaa vinavyopatikana katika mazingira yako ili liwe na gharama utakayoweza kumudu.
• Unaweza kutumia matofali ya udongo, udongo, miti, fito,n.k. Ukitumia fito au mabanzi ondoa maganda ili kuthibiti mchwa.
• Jengo mara litazuia maadui kama panya, vicheche, paka, nyoka na wezi kuingia ndani ya banda na kuwadhuru au kuwaiba kuku.
Liwe rahisi kusafisha
• Kuta na sakafu visiribwe zisiwe na nyufa ili kurahisisha kusafisha.
• Pia itadhibiti kusiwe na wadudu wa kujificha katika nyufa kama papasi, viroboto n.k.
• Sakafu ya banda lazima iwekewe matandazo kama pumba ya mpunga au maranda ya mbao au mabaki ya mazao au nyasi kavu kutegemeana na kinachopatikana kwa urahisi katika mazingira yako.
• Matandazo haya husaidia kunyonya unyevu unaotokana na kinyesi cha kuku au maji yanayomwagika katika banda.
• Banda hubakia kavu bila kuwa na harufu mbaya na wadudu kama inzi hata vimelea vya magonjwa hudhibitiwa.
Eneo la nje kuzunguka banda kuwe na usafi wa kudumu
Hali ya usafi nje ya banda itafanya wadudu kama siafu au mchwa na wanyama kama panya na paka mwitu wakose maficho. Nje ya banda ndani ya uzio kuwe na miti midogo na mimea mingine midogo kwa ajili ya kivuli.
Ufugaji nusu huria
Banda liwe na nafasi ya kutosha kwa kuku waliopo: Kwa kawaida eneo la mita mraba moja hutosha kuku wanne wanaotaga au kuku 8 wa nyama. Nafasi ya mita mraba 1 inatosha vifaranga 16 hadi kufikia umri wa majuma manne.
Liweze kuingiza hewa na mwanga wa kutosha: Banda linaloweza kuingiza hewa safi na kutoka ndani yake hubaki kavu. Harufu mbaya hutoka na kuku huweza kupumua hewa safi. Hii husaidia pia kudhibiti kuzaliana kwa vimelea vinavyosababisha magonjwa,hivyo hudhibiti magonjwa.
Lisiwe na joto sana au baridi sana: Panda miti ya kuzunguka banda lako ili eneo liwe na kivuli cha kutosha na pia lisiwe na upepo mkali.Kama hali halisi ya eneo la kufugia ina joto kubwa kwa vipindi virefu paa la banda wakati wa ujenzi liinuliwe juu zaidi kuruhusu mzunguko zaidi wa hewa na joto la paa ( kama ni la bati) liwe mbali juu ya kuku.
Joto kwenye banda linaweza kusababishwa na msongamano wa kuku, hivyo mfugaji aangalie aweke idadi ya kuku inayowiana na ukubwa wa banda lake.
Paa
Liwe imara na lisilovuja. Waweza kutumia mabati, nyasi, madebe, makuti n.k. kutegemeana na upatikanaji wa vifaa vya kuezekea.Wakati wa kuezeka paa lisiishie karibu sana na ukuta bali liwe na sehemu kubwa iliyozidi ukuta kuzuia mvua kuingia ndani kama ni ya upepo ( angalia mchoro hapa chini).
Vifaa vinavyohitajika katika banda la kuku
Kuku wakifugwa kwa mtindo wa nusu ndani na nusu nje wanahitaji huduma mbalimbali ndani ya banda na ndani ya wigo. Ili kutoa huduma hizi vifaa vifuatavyo ni muhimu viwe katika banda:
Vyombo vya Maji
Kuna njia nyingi za kutengeneza vyombo vya kuwekea maji ya kuku ya kunywa.
• Aina ya mojawapo unayoweza kutumia ndoo au debe la lita kumi au ishirini ya plastiki. Kata ndoo hiyo pande nne kutoa nafasi ya kuku ya kunywea kama kielelezo kinavyoonyesha. Tengeneza idadi ya vyombo hivi inayowiana na wingi wa kuku ulionao.
• Au waweza kutumia sufuria au beseni pana kiasi. Hii huwekewa tofali au jiwe safi pana baada ya kuwekewa maji ya kunywa ili kuzuia kuku wadogo wasizame na maji yasichafiliwe kirahisi.
• Vifaa maalum vya kunyweshea kuku vinapatikana katika maduka ya pembejeo za kilimo.
Vyombo vya chakula.
Vyombo hivi ni muhimu viwe vimetengenezwa vizuri ili visiwe chanzo cha upoteaji wa chakula. Unapotengeneza kilishio cha kuku kumbuka kuwa kuku wana tabia ya kuchakura. Husambaza au kupekua chakula kwa miguu hata kwa midomo ili kupata chakula cha chini.
Tabia hii husababisha kumwagwa kwa chakula kingi chini na kusababisha hasara. Unaweza kudhibiti tatizo hili kwa kutengeneza vyombo visivyoruhusu kuku kuchakura kama inavyoonyeshwa kwenye kielelezo hapa chini.
Unaweza kutengeneza kilishio hiki wewe mwenyewe au fundi seremala waliopo katika eneo unaloishi. Inafaa kilishio kiwe chembamba ili kuku wasiweze kuingia. Pia kinatakiwa kiwe kirefu ili kuku waweze kula bila kusongamana.
Viota
Zipo aina tofauti za viota ambazo hutumika kwa ajili ya kutagia. Ipo aina ya ambayo ni ya kutagia kuku mmoja mmoja. Vipimo vinavyopendekezwa kwa kila kiota ni upana wa sentimita 30, urefu sentimita 30 na kina sentimita 35. Upande wa mbele uachwe wazi ila sentimita 10 za kwanza kutoka chini zizibwe na ubao ( angalia kielelezo). Weka idadi ya viota inayotosheleza kuku ulio nao.
Pia ipo aina nyingine inayoweza kutumiwa na kuku zaidi ya mmoja kwa wakati mmoja. Ni kama kiota kimoja kilichogawanywa katika vyumba kadhaa. Ila kila chumba kina vipimo kama vya kiota kimoja( angalia picha hapa chini).Aina hii ya kiota ina upana wa sentimita 30 na kina sentimeta 35 na urefu wake unategemea idadi ya viota.
Viota vinatakiwa kuwa na giza ili kuku wasiogope kuingia kutaga ndani yake. Pia giza husaidia kupunguza tabia ya kuku kula mayai na kudonoana. Kiota kinafaa kuwekwa mahali ambako ni rahisi kuku kuingia na kutoka. Vile vile iwe ni sehemu itakayorahisisha usafishaji wa kiota chenyewe.
Kichanja.
Kuku wana asili ya kupenda kulala au kupumzika sehemu iliyoinuka. Hivyo ndani ya banda weka vichanja vitakavyotosheleza idadi ya kuku waliopo
Ulishaji: Kuku wa kienyeji wanaweza kulishwa kwa kumia mahindi, mchele, na mabaki ya ugali. Vyakula hivi ni lazima vikaushwe vizuri na kusagwa vizuri. Ulishaji ni lazima ufanyike katika sehemu safi au kwa kutumia vyombo vilivyotengenezwa maalumu kwa ajilii ya kulishia kuku. 
Banda: Kuku wawe wa kienyeji au wa kisasa, wanahitaji kuwa na banda zuri kwa ajili ya malazi na kuwalinda. Wanahitaji chumba chenye nafasi ya kutosha na kinachopitisha hewa ya kutosha. Ni lazima kuwawekea fito kwa kuwa ndege hupenda kupumzika juu ya fito. Ni lazima banda la kuku lifungwe vizuri nyakati za usiku ili kuzuia wanyama wanaoweza kuwadhuru kuku. Ni lazima liwe safi wakati wote ili kuzuia magonjwa kama vile mdondo na mengineyo. Usitumie pumba za mbao au nguo kuukuu kwenye viota vya kutagia kwani huchochea kuwepo utitiri na funza wa kuku. Inashauriwa kutumia mchanga laini.
Maji ya kunywa: Kuku wapatiwe maji safi. Ni lazima kuangalia mara kwa mara na kuyabadilisha maji. Kamwe usiwape kuku maji machafu.
Chanjo: Chanjo kwa mifugo ni lazima ili kuzuia mashambulizi ya magonjwa. Magonjwa yaliyozoeleka ni kama vile Mdondo, Kideri, Ndui ya kuku, na homa ya matumbo (typhoid). Chanjo kwa kawaida hutolewa mara moja kwa kila baada ya miezi miwili.
Uwekaji wa kumbukumbu: Kumbukumbu zijumuishe aina ya ulishaji, namba ya uzalishaji, muda wa mwisho wa matumizi, kiasi cha malisho kwa kila siku, idadi ya vifo, na idadi ya mayai yaliyozalishwa.
Mwanzoni unahitaji nini?
Wafugaji walio wengi wanauliza wanahitaji nini katika hatua za awali ili kuweza kuanzisha mradi wa ufugaji wa kuku. Hii itategemea aina ya kuku uliochagua kufuga.
Ni busara kuwa na vifaa muhimu vinavyohitajika na viwe katika hali ya usafi kabla ya kuweka kuku bandani mwako. Kama unaanza na vifaranga, vifuatavyo ni vifaa muhimu vinavyohitajika kwa ajili ya vifaranga 200.
• Tenga na utengeneze banda zuri lenye joto na hewa ya kutosha wakati wote.
• Vyombo vinne (4) vya kunyweshea maji, hii ni katika wiki 2 za mwanzo na uongeze vyombo taratibu kulingana na kuku wanavyokua.
• Vyombo vinne (4) vya kulishia chakula, na viongezeke kulingana na kuku wanavyokua.
• Matandazo makavu na safi, inaweza kuwa maranda au mabua ya ngano.
• Pakiti moja au mbili za dawa ya Coccid (hii inapatikana katika maduka yote ya kilimo). Hata hivyo, utaratibu wa chanjo ni lazima ukamilishwe.

• Chakula kwa ajili ya vifaranga ambacho kimezalishwa na watengenezaji wanaoaminika

Maelezo na ushauri zaidi wasiliana nasi :-

Tupigie kwa namba zetu 0769-457675 na 0678-226478
Au kupitia Whatsapp 0715-908307 na 0653-691138
Kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 11 jioni

No comments: